Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika uwanja huo Waziri Mshauri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Adel al-Jubeir amesema kuwa: "Iwapo miradi ya nyuklia ya Iran haitasitishwa Saudi Arabia itakuwa na haki ya kujizatiti kwa silaha za nyuklia."
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika jumuiya za kimataifa zenye makao huko Geneva, Kazem Gharib Abadi usiku wa kuamkia leo ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Iwapo Saudia ina mipango ya kutengeneza silaha za nyuklia au inatafuta kisingizio cha kuhalalisha hatua yake ya kukataa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki inapaswa kulipa gharama zake."
Gharib Abadi amemwambia Adel al-Jubeir kwamba: "Uzushi na kueneza hofu ni mbinu mbili zinazotumiwa kuwahadaa watu. Tafadhali msihusishe makosa yenu na pande nyingine zisizohusika."
Jambo la kuzingatiwa katika maudhui hii ni jinsi maafisa wa Saudi Arabia wanavyotumia madai ya uongo na yasiyo na msingi kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran kama wenzo na mwavuli wa kuficha na kuhalalisha shughuli za siri za nyuklia za utawala huo wa kifalme. Kwa maneno mengine ni kuwa, Wasaudia wanatayarisha mazingira ya kuelekea upande wa silaha za nyuklia, suala ambalo lina maana ya kuibua tishio na wasiwasi mpya wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia. Olli Heinonen aliyewahi kuwa naibu mkuu wa timu ya wakaguzi wa silaha za nyuklia wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Harvard anasema: "Saudi Arabia haijaweka wazi hata kidogo miradi yake ya nyuklia, na kama mfano tu nchi hiyo haijasaini protakali ziada ya wakala wa IAEA. Hadi sasa pia hatujaona mipango ya wazi ya nyuklia ya Riyadh ghairi ya kuainisha idadi ya mashinepewa zinazopaswa kutengenezwa. Vilevile katika mipango yao Wasaudia bado hawajachukua hatua yoyote ya kujenga vinu vya nyuklia."
Mwezi Agosti mwaka huu gazeti la New York Times liliandika ripoti kuhusu shughuli za siri za nyuklia za Marekani na kufichua uwepo wa chombo kikubwa karibu na taasisi za kuzalisha sahani za umeme wa sola (Solar Panel) katika eneo lililoko katika viunga vya Riyadh. Gazeti hilo lilifichua kwamba: Wataalamu wanadhani kuwa, chombo hicho ni sehemu ya vituo vya nyuklia ambavyo havijatangazwa na kuwekwa wazi na Wasaudia. Moja kati ya taasisi hizo yumkini ikawa ni ya kutayarisha keki ya njano iliyoko katika eneo la mbali la al "Alaa" huko Kaskazini Magharibi mwa Saudi Arabia.
Miaka miwili iliyopita mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman alianzisha mpango wa kuifanya nchi hiyo kuwa ya nyuklia kwa kuzindua miradi saba ukiwemo wa kinu cha nyuklia. Bin Salman alidai katika mahojiano yake na televisheni ya CBS kuwa, nchi yake haina mpango wa kumiliki silaha za nyuklia, lakini iwapo Iran itafanya hivyo, yeye pia pia hatasita kuwa na silaha za nyuklia!
Saudi Arabia inaendeleza miradi yake ya nyuklia kwa siri ilhali mkurugenzi wa zamani wa Wakala wa Kimataifa Wa Nishati ya Nyuklia, Yukia Amano, alisema mwishoni kwa kipindi cha uongozi wake kwamba, Saudia inapaswa kwanza kuruhusu ukaguzi wa miradi hiyo na taratibu nyingine za wakala huo kabla ya kuweka fueli ya nyuklia katika kinu kinachoendelea kujengwa huko Riyadh.
Kwa sasa kunajadiliwa swali kwamba, kumetukia kitu gani kilichowatia kiwewe na wahka maafisa wa Saudia kiasi cha kuanzisha tena propaganda chafu dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran? Sababu ya kukaririwa uongo huo dhidi ya Iran ni wasiwasi kuhusu mustakbali wa kisiasa wa maafisa hao wa Saudia hasa kwa kutilia maanani mwenendo wa sasa wa kuendelea kusambaratika udhibiti na ushawishi wa kisiasa, kiutamaduni na kijeshi wa Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.
342/